Tarehe 3 Novemba 2023

Tunawaalika wachapishaji, na wale wanaofanya kazi katika tasnia za uchapishaji kote duniani, wanaopigania haki, uhuru wa kusema, na nguvu ya neno lililoandikwa, kusaini barua hii na kujiunga na umoja wetu wa mshikamano wa kimataifa, Wachapishaji kwa Ajili ya Palestina.

Tunaheshimu ujasiri, ubunifu, na upambanaji wa Wapalestina, upendo wao wa kina wa ardhi zao za kihistoria, na uamuzi wao wa kutokubali kufutika, au kunyamazishwa, licha ya vitendo vya Israel vya kinyama na mauaji ya kimbari. Kinyume na njama za vyombo vya habari vya Magharibi na tasnia za kitamaduni, tuna matumaini kutokana na ongezeko la watu na vyombo mbalimbali, na sauti zinazoendelea kukusanyika, kuandika, kusema, kuimba, kupinga uwongo, na kujenga jumuia na mshikamano kupitia mitandao yote ya kijamii, na katika mitaa yetu, duniani kote.

Katika mwezi uliopita, tumeshuhudia mashambulizi mfululizo ya mabomu ya Israel huko Gaza kama adhabu ya pamoja, ikitumia mabomu ya fosforasi yaliyopigwa marufuku, na silaha mpya zisizofahamika, ikiungwa mkono na kupewa misaada ya serikali za Marekani, Canada, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Ulaya na Australia. Tumeshuhudia Wapalestina milioni 1.1 wakiyakimbia makazi yao kaskazini, kisha wakakumbana na uharibifu mkali wa hospitali na maeneo ya kimbilio kwenye shule, kambi za wakimbizi, makanisa, na misikiti kusini mwa Gaza. Kwa sasa, tunashuhudia watu milioni 2.3, asillimia 50% wakiwa watoto, wakinyimwa mahitaji ya msingi ya makazi, chakula, maji, mafuta, na umeme, wakati Israel ikifanya uvamizi wa ardhini. Zaidi ya Wapalestina 9,000 wameuawa hadi sasa, pamoja na vizazi vyote vya familia zilizoikimbia Gaza wakati wa Nakba ya 1948. Na kwa huzuni isiyovumilika, tumeshuhudia mauaji mabaya ya Israel ya zaidi ya watoto 3,500. Kama Raz Segal mwanafunzi Myahudi wa Holocaust na mauaji ya kimbari asemavyo: “Mshambulio ya kimbari ya Israel huko Gaza ni rasmi, wazi kabisa, na bila haya.”

Israel na mataifa ya Magharibi wanafanya jitihada za pamoja kuzima upinzani na kudumisha udhibiti wao unaoyumba. Katika tasnia za uchapishaji na vyombo vya habari tangu Oktoba 7, 2023, adhabu kwa kupaza sauti za kupinga yanayoendelea zimekuwa kali na nyingi. Tunalaani mauaji ya dazeni kwa dazeni za waandishi wa habari huko Gaza, ikiwa ni pamoja na Mohamed Fayez Abu Matar, Saeed al-Taweel, Mohammed Sobh, Hisham Alnwajha, Mohammad Al-Salhi, Mohammad Jarghoun, Ahmed Shehab, Husam Mubarak, Mohammad Balousha, Issam Bhar, Salam Mema, Assaad Shamlakh, Ibrahim Mohammad Lafi, Khalil Abu Aathra, Sameeh Al-Nady, Abdulhadi Habib, Yousef Maher Dawas, na Roshdi Sarraj.

Kama wafanyakazi wa kiutamaduni tunaotafakari kwa umakini maneno na lugha, tunakumbuka kuwa mauaji haya yalianzishwa na viongozi wa kijeshi wavamizi wa Israel wakitumia maneno kama “binadamu-mnyama,” kuhalalisha mashambulizi ya raia wakazi wa Gaza. Ni jambo la kutisha kushuhudia matumizi ya lugha ya kuumbua kama hiyo kutoka kwa watu ambao wenyewe walikwisha pitia hali hiyo katika muktadha wa mauaji ya kimbari. Pia tunakumbushwa lugha ya kufyeka watu kama majani na mauaji, iliyomo katika hadithi ya Kizayuni (na Kikristo) ya “Ardhi isiyo na watu kwa watu wasio na ardhi,” iliyotekelezwa na ukoloni wa Uingereza kwa kupitisha Azimio la Balfour, tarehe 2 Novemba 1917, miaka 106 iliyopita.

Historia hizi za kujiona bora kushinda watu wengine, ukoloni, na mifumo ya kibepari ya kuchimba, kutoa na kudhibiti, zinaonekana wazi katika kipindi cha sasa, hata ndani ya ulimwengu wa kipekee wa sanaa na utamaduni. Kuanzia kwenye kwa uamuzi wa uongozi wa Tamasha Maarufu la Vitabu la Frankfurt/Litprom kufuta tuzo iliyotolewa kwa mwandishi wa Kipalestina Adania Shibli (barua ya malalamiko dhidi ya hatua hii ilisainiwa na waandishi maarufu zaidi ya 1,000); kwa kuzuia mwandishi kama Viet Thanh Nguyen kusoma sehemu za maamdishi yake kule New York 92Y, na Mohammed el-Kurd katika Chuo Kikuu cha Vermont, na kufukuzwa kazi kwa David Velasco, Mhariri wa jarida la Artforum, mashirika ya kitamaduni na uchapishaji ya Magharibi yameonyesha jinsi yalivyoingizwa kichwakichwa katika masuala ya masilahi ya kisiasa na kiuchumi ya Marekani na Israeli kwa kuzima na kuadhibu waandishi wanaotetea na kuwasemea Wapalestina.

Tunalaani njama za wafanyakazi wote katika makampuni makubwa ya uchapishaji na kampuni za kujitegemea, wasioona ubaya wowote wa vitendo vya ugandamizaji kwa uoga wao, ukimya, na kwa kukubali njama za Israel na za mabeberu wafadhili wao, na watoa misaada ya fedha na serikali. Tunalaani kufuatafuata waandishi, na kudhibiti maadishi yao, vitisho na unyanyasaji wa wamiliki na wafanyakazi wa maduka ya vitabu, na vitisho vya wachapishaji wanaoshikamana na Wapalestina. Kwetu sisi, uchapishaji, ni zoezi la uhuru, kielelezo cha kiutamaduni, na upinzani. Kama wachapishaji, tunajitolea kujenga nafasi kwa ajili ya sauti bunifu za Kipalestina na za kisiasa, na kwa wote wanaosimama pamoja dhidi ya ubeberu,
uzayuni na ukoloni wa kilowezi. Tunatetea haki yetu ya kuchapisha, kuhariri, kusambaza, kushiriki, na kujadili kazi za ukombozi wa Palestina bila kulipiza kisasi. Tunajua kuwa hili ndilo jukumu letu katika upinzani.

Kunyamazisha waandishi wa Kipalestina kunaimarisha tu hofu ya upinzani wa kifasihi wa Kipalestina na kuchangia katika mauaji ya kimbari na wizi wa ardhi. Hofu ile ile iliyopo nyuma ya mabomu, uharibifu, utekaji nyara, na kuteswa kwa wafungwa wa Kipalestina, ndiyo hofu inayoshikilia nyaraka za Kipalestina zilizo chini ya udhibiti wa Israeli. Kama mwandishi Ghassan Kanafani alivyosema, “mapambano ya Wapalestina si mapambano ya Wapalestina pekee, bali ni mapambano ya kila mwanamapinduzi.” Anatukumbusha kuwa hakuna kati yetu anayeweza kuwa huru hadi sote tuwe huru.

Sasa ni wakati wa kusimama kidete na Wapalestina na kuingia katika enzi mpya ya kupinga ukoloni – enzi inayokataa makubaliano ya Oslo na uhusiano wa kawaida na dola la Kizayuni. Sasa ni wakati wa kukumbuka na kudumisha ushindi katika mapambano ya kihistoria dhidi ya tawala za kilowezi, kama vile upinzani ulivyoikomboza Algeria kutoka kwenye ukoloni wa Wafaransa. Sasa ni wakati wa kuongeza nguvu katika kuunga mkono ukombozi wa Palestina kutoka kwa Israel na wafadhili wake wa Amerika na Ulaya. Sasa ni wakati wa kujenga mshikamano kati yetu ili kwa pamoja tukatae vitisho, ukandamizaji, hofu, na vurugu za mapigano.

Tunawakaribisha makomredi, marafiki, na washirika wenzetu katika tasnia mbalimbali za uchapishaji kuweka saini zao kwenye waraka huu na kuunga mkono madai yafuatayo:

  • Sitisha mauaji ya kimbari na maliza vurugu zote dhidi ya Wapalestina huko Gaza, Ukingo wa Magharibi, kote katika Palestina ya kihistoria, na katika diaspora.
  • Wawajibishe Israel na washirika wake wote kwa makosa ambayo wamefanya ya jinai ya kivita.
  • Unga mkono madai ya Wapalestina ya uhuru, haki ya upinzani, na kurejea kwao.
  • Unga mkono wito wa kususia, kusitisha uwekezaji na kuuwekea vikwazo (BDS) utawala wa Kizayuni.
  • Hakikisha kuwa sauti za Wapalestina hazizimwi kwenye maonyesho ya kimataifa ya vitabu na tamasha za fasihi duniani. Badala yake, wanapaswa kualikwa kama wageni wa heshima kushiriki na kusimulia hadithi zao.
  • Jitolee kwa dhati kufanya tasnia ya uchapishaji kuwa mahali huru pa kujifunza na penye uhuru wa kusema. Kama wachapishaji, tunajitolea kutenga nafasi kwa ajili ya sauti za Wapalestina na wale wanaosimama pamoja nao dhidi ya mashine ya vita.

Imesainiwa na: [Majina yanasubiriwa]